Mkuu wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Dkt. Ahmed Omar amempa mwalimu mkuu wa shule ya Tot hadi Jumatatu wiki ijayo kuhakikisha wanafunzi wote wanaenda shuleni na kurudi nyumbani.
Mkuu huyo alikerwa na hatua ya mwalimu huyo kuifanya shule hiyo kuwa ya bweni ilhali imesajiliwa kama shule ya kutwa huku wanafunzi wakiishi kwa mazingira duni.
Omar alishangaa shule hiyo ambayo ni ya mseto haina bweni na wanafunzi wamelazimika kulala sakafuni kwa vyumba vya muda akiongeza kwamba wanafunzi 1,100 wanatumia vyoo vinne tu.
Mkuu wa shule hiyo Lawrence Mutwol alijitetea kwamba alichukua hatua hiyo kutokana na visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo ambalo lilikuwa linashuhudia ghasia za wizi wa mifugo akisema shule hiyo iliwapoteza wanafunzi wawili mwaka jana kwa ghasia hizo.
Aliendelea kusema alifanya hivyo kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi waliojiunga na shule hiyo kutokana na sera ya serikali ya kuhakikisha wanafunzi wote wa darasa la nane wanajiunga na shule ya upili.
Mutwol alisema wanatarajia kupata vitanda 200 wiki hii kutoka kwa wahisani wawili, kwamba wana mipango ya kujenga vyoo zaidi akiongeza wako katika harakati za kusajili shule hiyo kama shule ya bweni.
Hata hivyo mkuu wa kaunti alisema hajaridhishwa na maelezo hayo akisema bodi ya usimamizi wa shule hiyo ingeweka mikakati inayofaa kabla ya kuwachukua wanafunzi wa bweni.
“Siwezi kubali wanafunzi kuishi kwa mazingira kama haya ambayo hayafai kabisa kwa masomo. Masomo hayaendelei tu darasani bali mazingira yanachangia pakubwa na kwa hivyo nawapa hadi jumatatu kuhakikisha shule hii imebaki kuwa ya kutwa,” alifoka Omar.
Alishangazwa pia na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo ikilinganishwa na shule zingine jirani akisema wanafunzi wengine wanafaa kupelekwa kwa shule jirani ili kupunguza msongamano katika shule ya Tot.
Mkuu huyo alimuagiza mkurugenzi wa elimu katika kaunti, Kituyi Masibo kuwatuma wakaguzi wa mahesabu katika shule zote katika kaunti kuona fedha zinazotumwa na serikali kugharamia elimu zinatumiwa kwa njia inayofaa.
Pia aliwataka maofisa wanaosimamia ubora kukagua shule zote ili kuona kwamba wanafunzi wanasoma kwa mazingira yanayofaa.
Masibo alisema mwalimu huyo na bodi yake walikiuka sheria ya elimu ya msingi kwa kuifanya shule hiyo kuwa ya bweni ilhali imesajiliwa kuwa ya kutwa.
Na Alice Wanjiru