Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Vihiga > Biwi la simanzi latanda Vihiga, kuomboleza vifo vya wahubiri, Mombasa

Biwi la simanzi latanda Vihiga, kuomboleza vifo vya wahubiri, Mombasa

Hali ya huzuni imetanda katika kijiji cha Chango Kaunti ndogo ya Vihiga kutokana na kifo cha mhubiri mmoja na bibiye kilichotokea katika Kaunti ya Mombasa.

Inasemekana mhubiri huyo anayefahamika kama Elisha Misigo alimuua bibiye, Hannah Maganga walipokuwa kanisani siku ya Jumapili na kisha akajitoa uhai.

Margret Nandoya, mamake mhubiri huyo, ameelezea kutamaushwa kwake na kitendo alichokifanya mwanawe ambaye amemtaja kama mtu aliyefuata kwa karibu sana kanuni za kikristo.

Nandoya, ambaye hangeweza kuzuia machozi, alisema kwamba marehemu na bibiye wamekuwa wakiishi kwa amani baada ya arusi yao. Hata walikuja nyumbani hivi karibuni kuwatembelea.

Hata hivyo, mama huyo alifichua kwamba kulikuwa na migogoro kidogo kidogo ya kifamilia kati yao wawili iliyotokana na umiliki wa kanisa lao. Inasemekana kwamba migogoro hiyo hata ilisababisha kutengana kwao mwaka uliopita.

“Kijana wangu vile alienda Mombasa kutafuta kazi alikuwa anajiwekea pesa kidogo kutoka kwa malipo aliyoyapata kisha akanunua ploti ambapo alijenga kanisa. Fedha waliyoipata kutoka kwenye kanisa hilo naelewa ndiyo iliyoleta shida,” alinena.

Hata hivyo, washiriki wa kanisa hilo wamelaumiwa kwa kukosa kusuluhisha migogoro hiyo kwa wakati unaofaa, jambo ambalo lingeepusha kisa hicho.

Jirani wao, Esther Mung’ora, amemtaja marehemu Elisha kama mtu mzuri ambaye alikuwa anatoa mfano mwema kwa vijana huku akishindwa kuelewa kile kilichotokea na kumfanya achukue hatua ya kumuua bibiye na kisha kujitoa uhai.

Marehemu wamewaacha watoto wanne ambao wamekuwa wakiishi na mama yao tangu mwaka jana wakati migogoro hiyo ilipoanza.

Na  Isaiah Nayika

Leave a Reply