Wajumbe zaidi ya 1100 wanasikiliza kwa makini wakiwa wameketi katika mahema mawili. Huku ameshika mkononi nakala ya atakayonenea kwa muhtasari na baadhi yao kutumia chombo cha elektroniki, msemaji mmoja baada ya mwingine anakwenda jukwaani kuzungumzia somo fulani. Kufuata wakati ni muhimu sana. Kila msemaji anajitahidi kuwa makini asipitishe muda aliopewa.
Alasiri inafika. Msemaji mmoja miongoni mwa wasemaji wengine anaelekezwa jukwaani. Nakala za habari fupi alizoshika mkononi ni nene kuliko za wasemaji wengine waliomtangulia. Watakaomfuata pia hawatakuwa na taarifa ndefu kama yake. Msemaji huyu haoni. Jina lake ni Gilbert Kamande. Yeye ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Gakoigo, huko Maragua.
Pale anapofanya kazi, anafundisha Masomo ya Jamii, lugha ya Kiswahili, au Elimu ya Dini ya Kikristo. Lakini kwenye siku ya leo, Agosti 18, 2023, habari ya Biblia ndilo somo hasa la hotuba inayotolewa kwa lugha ya Gikuyu.
Hii ni siku ya kwanza kati ya zile tatu za Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova “Kuweni na Subira”. (“Onanagia Wetereri”! Kigomano kía Aira a Jehova kía 2023) Mahali pa kusanyiko ni Havila Resort huko Sagana.
Maelezo yake Kamande yamenakiliwa kwa maandishi ya breli, inayoandikwa kwa mchanganyiko wa vidutu sita. Anapaswa kuwasomea wasikilizaji angalau andiko moja. Lakini anasoma mawili.
“Sikuweza kuibeba Biblia yangu kwa sababu ni kubwa sana,” anaeleza. “Mwanangu Jolys alinisomea maandiko hayo. Nikayaandika kwa breli katika muhtasari na kuwasomea wasikilizaji pale jukwaani.”
Biblia ya Kamande si ya kawaida, yake ni Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko Matakatifu, ikiwa katika breli ya daraja la pili, yenye mabuku 24. Kila moja ina ukubwa wakulinganishwa na encyclopaedia. Iko hivyo kwa sababu maandishi ya breli ni makubwa.
Kamande anavithamini sana vidole vyake kama wale wanaoona wanavyothamini macho yao. Kwa kutumia ncha za vidole vyake, anaupitia muhtasari wake kwa ajili ya mambo ya kuzungumza huku akiendelea kuwahutubia wasikilizaji wanaosikiliza kwa makini. Anadumisha uhusiano wake na wasikilizaji ingawa hawezi kuona jinsi wanavyoitikia.
Anavifuatilia vidutu kwa kutumia mkono wake wakulia akisonga kuelekea upande wa kulia wa ukurasa. Mkono wake wakushoto unatumika kufuatilia mstari unaofuata katika mpangilio wa maandishi. Katika muda aliopewa anamaliza sehemu yake. Kisha wasikilizaji bila kutazamia wanapiga makofi huku akishuka toka jukwaani akiandamana na mwelekezi wake.
Mkewe Beth Wangui, binti Irene Waithira, 21 na mwanaye wa kiume Jolys Githuku, 17 wanaungana na Kamande kwa muda uliobakia wa ratiba. Githuku alimsaidia kupima wakati alipokuwa akifanyia mazoezi hiyo sehemu yake.
“Baba yangu hajawahi kuniona,” Githuku anasema. “Nyakati zingine mimi husahau kuwa yeye ni kipofu kwa sababu yeye ni mfanyakazi mwenye bidii.”
Programu zilizochapishwa na za kielektroniki katika simu au kishikwambi zimesambazwa kwa wajumbe. Programu ya Kamande inapatikana katika breli. Ndio programu iliyo kubwa kuliko zote katika kusanyiko hili lote. Lakini hilo halimsumbui akili.
Alitumia programu hiyo ya breli kuchochea hamu yake kwa ajili ya kusanyiko kabla hajafika hapa katika eneo hili zuri la kusanyiko. Tayari siku tatu zimepita na hayuko gizani asijue ni kipi kitakachofuata baada ya hapo.
Kila siku ina kichwa chake cha maaandiko. Muda wa kuanza na kumalizika kwa programu ya kila siku umeonyeshwa. Nyimbo zitakazoimbwa zimewekwa humo. Picha za programu zina maelezo ya kumwezesha Kamande kutafakari kilichomo katika picha.
“Tulihakikisha kuwa tumesoma maandiko yote yaliyotajwa katika programu hii ili tukifika hapa tufaidike na programu,” anasema. Uwezo wa Kamande wa kusikiliza umeboreshwa zaidi. Mke wake Wangui anasema, “Mara nyingi yeye anasikiliza na kuelewa zaidi kuliko sisi tunavyosikia na kuelewa.”
Mojawapo ya changamoto ni kuhusiana na video zilizo na vitendo visivyo na sauti, Anahitaji msaada hapa, “Ninapata maelezo kuhusu kinachofanyika kutoka kwa wale walio karibu yangu.” anafafanua.
Familia ya Kamande imekuwa ikilitazamia kwa hamu sana kusanyiko hili. Ni la kwanza kufanyika ambapo wajumbe wamekutana ana kwa ana tangu janga la COVID-19 lilipozuka.
Noah Munyao ambaye ni msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Kenya anasema: “Jumla ya makusanyiko 35 yamepangwa kufanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo, Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru, Machakos, Sagana na Embu. Kisha anaongeza, “Yatafanyika kwa kuwasiliana kupitia Kiswahili, Kikamba, Kikuyu, Kiingereza na Lugha ya Alama ya Kenya.”
Makusanyiko 6000 hivi yatafanyika ulimwenguni kote kama sehemu ya mfululizo wa makusanyiko ya 2023 ya “Kuweni na Subira!”
“Ingekuwa vyema kupata nakala ya hotuba kama watu wengine wanaoona,” Kamande anasema. “Inachangamsha moyo wangu sana kuona kuwa watu kama sisi hatujapuuzwa.”
Matayarisho yenye uangalifu mkubwa yanahitajiwa katika hotuba kama ambayo Kamande ameitoa. Inahitaji kufanya utafiti katika vyanzo mbalimbali vya habari. Jambo la kufurahisha ni kuwa breli ya Kamande ina habari zaidi ya zile za Biblia.
Katika chumba chake cha kujifunzia Kamande ametenga rafu kadhaa kwa ajili ya Biblia yake. Biblia yake inafikia kimo cha karibu futi saba inapopangwa moja juu ya nyingine.
Alianza kupokea visehemu vya maandiko haya katika mwaka wa 2021. “Kila baada ya miezi mitatu mabuku mawili au matatu yaliletwa kwangu kutoka Ofisi ya Tawi ya Mashahidi wa Yehova iliyoko Nairobi mpaka wakati mabuku yote yalipokuwa yamekamilika,” anakumbuka.
Biblia yake ina vitabu 66 tokea Mwanzo hadi Ufunuo. “Napendelea kusoma Biblia yangu mapema sana asubuhi kunapokuwa kimya,” anasema. “Kuwe na umeme au la hilo kwangu si kizuizi.”
Kamande anaufahamu mpangalio wa chumba chake cha kujifunzia. Anajua kuchomoa buku analolitaka. Baada ya funzo analirudisha palepale alipolichomoa bila kukosea.
Kabla hajapata hiyo Biblia yake ya breli, alisikiliza Biblia iliyorekodiwa. Njia nyingine aliyotumia ni kusomewa visehemu vya Biblia kwenye Biblia ya kawaida.
“Pia ninapokea machapisho mengine ya kujifunzia Biblia katika breli,” anasema. “Hayo huletwa katika Jumba letu la Ufalme la Maragua.”
Kamande hakuzaliwa akiwa kipofu. Macho yake yalianza kudhoofika alipokuwa na umri wa miaka 12. Hivyo wazazi wake walimpeleka katika Shule za Msingi na Sekondari za Thika kwa ajili ya vipofu. Hizi ndizo shule zilizomfundisha daraja la kwanza na la pili la breli.
Jitihada inahitajika kujifunza breli. Kuwa na subira kunahitajiwa pia. Kamande alistawisha sifa hizi. Matokeo yake ni kuwa alielewa vifupisho vya maneno na sasa hakuna neno la Kiingereza asiloweza kusoma au kuandika katika breli.
Siku tatu alizozitumia pamoja na familia yake katika kusanyiko hili anasadiki kuwa zitamsaidia kuwa na subira katika midani nyingine za maisha yake.
Na William Inganga